Mnamo Desemba 17, 2022, Metropolitani Leonid wa Klin, Askofu Mkuu wa Afrika, alihudhuria tamasha la muziki wa Kirusi, lililofanywa na kikundi cha muziki cha Mosko kiitwacho “Vera” (Mkurugenzi wa Sanaa – Evgenia Kuznetsova).
Tamasha hilo, lililofanyika katika Kanisa Kuu la Kikatoliki la Mtakatifu Petro, lililoko katika uwanja wa Julaian, katikati mwa mji mkuu wa Moroko, liliandaliwa kwa msaada wa Ubalozi wa Urusi nchini Moroko na “Jumba la Urusi” mjini Rabat.
“Leo tumekusanyika hapa katika hafla ya ziara ya kwanza ya Askofu Mkuu wa Afrika hapa Moroko kwa adhama ya miaka 90 ya kuanzishwa kwa Kanisa letu la Kiothodoksi la Ufufuo wa Kristo,” Metropolitani Leonid alisema katika hotuba yake ya ufunguzi, akinukuliwa. na TASS. Askofu huyo alikumbusha kwamba katika mwaka huu pia kunaadhimishwa miaka 100 ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, na akamshukuru Askofu Mkuu wa Jimbo la Rabat, Kadinali Kristobal Lopez Romero, kwa kuwezesha uandaaji wa tamasha katika kanisa hilo.
Miongoni mwa waalikwa walikuwa Balozi wa Urusi nchini Moroko Vladimir Baibakov, wafanyakazi wa uwakilishi wa kidiplomasia wa Urusi na taasisi-wakilishi nyingine, wawakilishi wa jumuiya ya wazungumza- lugha ya Kirusi ya mjini Rabat na pia raia wa Moroko.
Programu ya tamasha ilijumuisha nyimbo za kiroho za watunzi wa Kirusi, nyimbo za Krismasi zikiwa katika lugha mbali mbali, nyimbo maarufu za asili na pia za watunzi.
“Asante sana kwa zawadi hii ya Krismasi, ambayo ni hili tamasha la leo,” Kadinali Kristobal Lopez Romero alisema katika kuhitimisha, akionyesha matumaini kwa ushirikiano zaidi katika siku za usoni.
Metropolitani wa Klin Leonid, kwa upande wake, aliwapongeza Wamoroko kwa timu yao ya taifa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Dunia nchini Qatar.
Kanisa la Ufufuo wa Kristo kule Rabat ndilo kanisa kongwe zaidi la Kiothodoksi la Urusi barani Afrika. Kuanzia Desemba 29, 2021 – limewekwa chini ya mamlaka ya Dayosisi ya Afrika Kaskazini ya Patriarkia ya Mosko.