Metropolitani Leonid: Hali ya Wakristo katika Bara la Afrika inazorota                                 - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Metropolitani Leonid: Hali ya Wakristo katika Bara la Afrika inazorota                                

Mashirika yanayojinasibu kuwa  ni ya kupigania haki za binadamu yanafumbia macho matukio ya kutisha yanayojili barani Afrika, ambapo hali ya wakristo inazidi kuwa tete, Askofu Mkuu wa Afrika Metropolitani wa Klin Leonid aliiambia Sputnik.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, kiwango cha mateso ya wakristo ulimwenguni kimeongezeka sana katika miaka 30 iliyopita. Katika bara la Afrika, hususan eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara, hasa Nigeria, hali ni mbaya zaidi. Tatizo hili limejulikana kwa muda mrefu, na kiwango chake kinazidi kuwa kibaya. Kwa nini inashindikana kuidhibiti hali hiyo?

— Hakika, katika miaka ya hivi karibuni na miongo kadhaa, hali ya wakristo katika bara la Afrika  (Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara) imekuwa mbaya zaidi. Licha ya ukweli kwamba idadi ya wakristo katika eneo hili inaongezeka kwa kasi, bado wanakabiliwa na vitisho pamoja na mateso mengi, na Nigeria ndiyo nchi ambako mateso ya wakristo ni makubwa zaidi. Kila mwezi, na karibu kila wiki, wakristo wanauawa kwa sababu  za kidini. Kwa nini hali hiyo haidhibitiwi? Kwani, kwa maoni yetu, ili kutatua tatizo hili, kwanza kabisa, ni lazima kukabiliana na ukweli, kwa uwazi na kwa uaminifu kabisa, katika ngazi zote – kimataifa, kitaifa i – kwamba haya ni mauaji ya kimbari ya wakristo, ni vita vya kiimani, na si vya migongano ya kisiasa au  ya kitaifa au kijamii, kama baadhi ya wachambuzi wanavyojaribu kufikiria. Haya ni mashambulizi kwa misingi ya kidini, mashambulizi ya imani, na mpaka ukweli huu utakapokuwa wazi kwa kila mtu, hadi tasnifu hii itakapokuwa mada ya majadiliano na kisababishi cha maamuzi madhubuti, hali haitabadilika. Na tusipolizungumza waziwazi tatizo lililopo, huku tukiita vitu kwa majina yao halisi, tatizo hili halitatatuliwa kamwe. Hivi sasa hali hii inaathiri si Nigeria tu, bali pia baadhi ya maeneo ya nchi jirani za Niger, Kamerun, Mali, na Burkina Faso. Ichukuliwe tu kwamba mamlaka zinazonufaika kutokana na vurugu katikati pamoja na magharibi mwa Afrika, zinayatumia matatizo yaliyopo kaskazini mwa Nigeria katika muktadha wa mapambano baina ya dini.

Ni hatua gani, kwa maoni yako, zinahitajika ili kuwalinda vyema wakristo katika Afrika na Mashariki ya Kati?

— Kanisa la Kiothodoksi la Urusi lina maono ya wazi na jibu la wazi kwa swali hili. Patriarki Mtakatifu Kirill, mwanzoni kabisa mwa kile kinachoitwa “Arab Spring”, alipotembelea Syria, alibainisha kwamba kazi muhimu zaidi ya viongozi wa dini ulimwenguni kote, ni kuufikisha ukweli kwa jumuiya ya dunia nzima kuhusu hali ya wakristo wanakoteswa, si kuachia mambo kwa wepesi wepesi tu, si kufumbia macho kile kinachoendelea, bali bila kuchoka, kupaza sauti kwa kutumia  mikutano mikubwa yote kwa kadri iwezekanavyo, na hata. majukwaa makubwa zaidi ya kimataifa, kuanzia na Umoja wa Mataifa na kumalizia na mashirika makubwa ya huduma za kibinadamu, na ya kulinda amani kwenye sayari yetu hii. Hii ni hatua ya kwanza katika kuelekea kuwalinda wakristo barani Afrika na pia Mashariki ya Kati.

Hatua inayofuata ni wito wa kuchukua hatua madhubuti, za kuungana katika juhudi za kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakristo – wahanga, huduma ambayo Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika  inajishughulisha nayo.

Wakati huo huo, hatua  stahiki zinapaswa kuchukuliwa ili mauaji ya kimbari ya wakristo yasitumike kama kigezo cha kisiasa katika kuzidisha hali ya vurugu katika baadhi ya nchi, kubadili tawala za kisiasa. Ni muhimu sana kutambua kwamba ni vema kushirikisa si tu mamlaka za kisiasa, za ndani,  bali pia kwa wadau wa nje ambao sasa wanaingilia hali ilivyo katika nchi nyingi na kutumia kigezo cha udini kwa manufaa yao wenyewe. Kwa uhalisi haya yanatokea katika nchi zote za Afrika ambako wakristo wanateswa, na si Nigeria pekee.

Jumuiya ya kimataifa inafuatilia kwa karibu utetezi wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi. Uhalifu wa kutisha dhidi ya wakristo unafanyika Afrika na Mashariki ya Kati. Je, tatizo hili linazingatiwa vya kutosha na jumuiya ya kimataifa?

— Kama ilivyoelezwa tayari, kuna utofauti mkubwa kati ya kuzingatia kwa mashirika ya kimataifa, hata yenye mamlaka zaidi, kama vile Umoja wa Mataifa, kwa swala la kuheshimu haki za binadamu katika nchi za Magharibi, kwa mada- sawia ya Ukraina, ambayo leo haiishi kuwa agenda ya wazungumzaji wenye ushawishi mkubwa duniani, kama tujuavyo, wakitoa habari za upande mmoja, na kwa hali ya watu wa Afrika na Mashariki ya Kati. Mashirika ambayo yanajinasibu kuwa  ni watetezi  wa haki za binadamu yanafumbia macho matukio ya kutisha yanayojili katika eneo hili, ambapo hali ya wakristo ni tete sana.

Kile ambacho bado kinatokea Syria, Iraki na Yemen kinaweza kuitwa janga la wakristo pamoja na vikundi vingine vya raia, ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi. Wakati huo huo, hakuna chochote kinachosikika kuhusu jambo hili kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa, na taarifa kuhusu hilo huonekana mara chache sana. Hakuna kinachosemwa kuhusu Yemen; ilhali vita ingali imepamba moto, njaa na kutoweka kwa idadi kubwa ya watu, kutokana na matukio haya, kunaendelea. Na  kama tunazungumza kuhusu Afrika, ambayo iko katika uangalizi wetu wa moja kwa moja, basi tunaweza kuorodhesha pengine nusu ya nchi za bara hilo. Hii itakuwa orodha ndefu sana ya uvunjifu wa kutisha wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unayofanywa kwa misingi ya dini, mateso ya watu kutokana na uhaba wa chakula, ambao unatengenezwa na nchi za Magharibi na hapa tunaongelea kuweka vizuizi vya usambazaji wa nafaka kutoka Urusi, au kwamba  nafaka hizi zitaanza tena kusafirishwa. Imetangazwa kuwa Afrika itapatiwa chakula, na chakula hiki chote kimehifadhiwa mahali fulani kule Ulaya na kuwa mawindo ya mawakala wa Ulaya hiyo hiyo, wakijihusisha na udalali wa chakula, mbolea, nk. Ghilba kwa matatizo ya Afrika na mahitaji yake inafanyika. hata katika ngazi ya kimataifa kama hii.

Lakini, nikizungumzia ukweli kwamba nchi nyingi za Kiafrika zinaweza kuorodheshwa katika mfululizo huu wa nchi zenye matatizo ambapo haki za binadamu zinakiukwa, ningependa kwanza kabisa kujielekeza si  kwenye ukweli kwamba nchi hizi, zenyewe zina kasoro fulani katika miundo yao ya ndani. Hatukosoi mamlaka ya nchi fulani fulani katika suala hili, kwa sababu kama tunazungumzia matatizo ya Afrika, basi hayo yanaunganishwa na ukweli kwamba, kwa sehemu kubwa, yanasukumwa kutoka nje. Tusisahau ukweli kwamba Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa wa raslimali. Hili ndilo bara ambamo kunapatikana madini, ambayo bila uwepo wake,  viwanda vikubwa, ikiwa ni pamoja na vya tasnia ya “IT”, visingekuwapo. Afrika ni bara ambalo nguvu-kazi yake inatumika kiunyonyaji tu. Hii ni nguvu kazi ya bei rahisi sana, kwani ili wasife kwa njaa, watu hawa wanalazimika kufanya kazi katika migodi isiyo na mazingira –rafiki, yasiyofaa, yisiyovumilika. Ili kuwaweka waafrika katika hali kama hiyo, bila shaka, ghiliba zinazoendana na kuzidisha machungu katika nchi-husika, vita, machafuko ya ndani, hasa kwa misingi ya dini, inahitajika. Ni rahisi sana “kuvua samaki katika maji ya matope”, jambo ambalo mashirika makubwa ya kimataifa yanafanya, kwanza kabisa kwa kutumia raslimali za Afrika kujitajirisha. Hilo ndilo tatizo kuu. Bila shaka, hii haitiwi maanani na jumuiya ya kimataifa. Zaidi ya hayo, uchambuzi wa kina wa hali hiyo unaweza kupelekea kwenye hoja kwamba, jumuiya ya ulimwengu ulioendelea inatumia matatizo ya Afrika kwa manufaa yake. Leo hakika tuko katika hatua hii ya mjadala wa matatizo ya Afrika. Mungu ajalie tufikie  wakati ambapo hali ya waafrika kutumiwa na wababe wa dunia, kwa malengo yao, ikome. Kwa upande wetu, tunachukua na tutaendelea kuchukua hatua zote zinazostahili ili kuwalinda wakristo na kusaidia wakazi wa nchi za Afrika.

Shirikisha katika mitandao ya kijamii: