Misingi ya Mafundisho ya Kanisa kuhusu Familia na Malezi ya Mtoto: Mila na Usasa - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Misingi ya Mafundisho ya Kanisa kuhusu Familia na Malezi ya Mtoto: Mila na Usasa

Mnamo tarehe 27 Julai, 2023, Askofu Mkuu wa Afrika, Metropolitani wa Klin Leonid, alitoa hotuba juu ya “Misingi ya Mafundisho ya Kanisa kuhusu Familia na Malezi ya Mtoto: Mila na Usasa” katika kikao cha “Ushirikiano katika eneo la ulinzi wa haki za watoto: mwelekeo wa maendeleo na aina za ushirikiano”,kilichoandaliwa chini ya mwavuli wa Mkutano wa Pili wa Kilele wa Urusi-Afrika.

Wapendwa kaka na dada zangu!

Bwana wetu Yesu Kristo anasema: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa mbinguni ni wao” ( Matayo 19:14 ). Pia anatabiri hatima isiyozuilika kwa wale wanaopandikiza majaribu na kuleta uharibifu kwa roho dhaifu za watoto: “Ila yeyote atakayemshawishi mmoja wa wadogo hawa, wanaoniamini, ingekuwa heri kwake kama angefungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kilindi cha bahari” (Matayo 18:6).

Ukristo ulizijaza fikra za kipagani na za Agano la Kale kuhusu ndoa ,na sura ya muungano wa Kristo na Kanisa. Kwa Wakristo, ndoa imekuwa siyo tu mkataba wa kisheria, nyenzo ya kuridhisha mahitaji na hisia za muda mfupi tu, bali, kwa kauli ya Mtakatifu Yohana Zlatousti, “ni sakramenti ya upendo”, ni muungano wa milele wa wanandoa, katika Kristo.

Kanisa linasisitiza juu ya uadilifu katika maisha yote ya wanandoa na kutovunjika kwa ndoa ya Kikristo.

Klementi wa Aleksandria anaiita familia kuwa ni Kanisa, Makao ya Bwana, huku Mtakatifu Yohana Zlatousti akiita familia kuwa ni “kanisa dogo”. “Niseme tena,” anaandika mtumishi wa Mungu, “kwamba ndoa ni mfano wa Kanisa.” Kanisa la nyumbani linaundwa na mwanamume na mwanamke, wanaopendana, waliounganishwa katika ndoa na kuadama kwa Kristo. Matunda ya upendo wao na jumuiya ni watoto, ambao kuzaliwa kwao pamoja na malezi yao, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiothodoksi, ni kati ya malengo muhimu sana ya ndoa.

“Huu ndio urithi utokao kwa Bwana, wana; zawadi kutoka kwake – matunda ya tumbo la uzazi,” Mtunga Zaburi anapaza sauti (Zab. 126:3). “Watoto hawapatikani kwa bahati mbaya, tunawajibika kwa wokovu wao .. Kupuuza watoto ni dhambi kubwa kuliko dhambi zote, husababisha uharibifu uliopitiliza … Hatutakuwa na kisingizio endapo watoto wetu wataharibika,” Mtakatifu Yohana Zlatousti alisema. Mtawa Efraimu Mshami anafundisha: “Heri yeye aleaye watoto wanaompendeza Mungu.” “Waheshimu baba yako na mama yako, siku zako zipate kuwa nyingi duniani,” inasema amri ya tano ya Torati ya Musa (Kutoka 20:12).

Familia, kama kanisa la nyumbani, ni kiumbe kimoja, ambacho washiriki wake wanaishi na kujenga uhusiano wao kwa msingi wa sheria ya upendo. Uzoefu wa mawasiliano ya familia hufundisha mtu kushinda ubinafsi wa dhambi na kuweka misingi ya uraia, yenye afya. Ni katika familia, kama katika shule ya uchamungu, ambapo mtazamo sahihi kwa majirani wa mtu hutengenezwa na kuimarishwa, na kwa hiyo, kwa ndugu wa mtu huyo na kwa jamii kwa ujumla. Mwendelezo wa maisha, wa vizazi, kuanzia familia, hupata mwendelezo wake katika upendo wa wahenga, kwa maana ya kuwa mali ya historia. Kwa hiyo, ni hatari sana kuharibu mahusiano ya asili kati ya wazazi na watoto, ambako, kwa bahati mbaya, kunafanywa, kwa kiasi kikubwa, na hali ya sasa ya maisha ya jamii.

Uyatima katikati ya wazazi walio hai umekuwa msiba wa kutisha kwa jamii ya leo. Maelfu ya watoto waliotelekezwa wanajaza vituo vya kulelea , na wakati mwingine wanaishia mitaani, na ni ushuhuda wa hali mbaya ya jamii. Kwa kuwapatia watoto hao msaada wa kiroho na kimwili, kuendeleza ushiriki wao katika maisha ya kiroho na kijamii, Kanisa linadhihirisha uwajibikaji wake katika kuimarisha familia na ufahamu wa wazazi juu ya wito wao, ambao utaondoa janga la kutelekeza watoto.

Propaganda za maovu husababisha madhara makubwa kwa nafsi za watoto na vijana. Katika vitabu, filamu na bidhaa zingine za video, katika vyombo vya habari, na vile vile katika programu zingine za kielimu, vijana, mara nyingi huvutiwa na wazo kama la mahusiano ya ngono, ambayo ni ya kudhalilisha utu wa mtu, kwani ndani yake hakuna dhana ya usafi wa kiroho, uaminifu katika ndoa na upendo usio na ubinafsi. Kanisa linawataka waumini, kwa kushirikiana na mamlaka zote zenye afya ya kimaadili, kupambana dhidi ya kuenea huku kwa majaribu haya ya kishetani, ambayo yanachangia katika kuharibu familia na kudhoofisha misingi ya jamii.

Kwa kutambua kwamba shule, pamoja na familia, inapaswa kuwapa watoto na vijana ujuzi juu ya uhusiano wa jinsia na juu ya asili ya mwili wa mwanadamu, Kanisa haliwezi kuunga mkono mipango ya “elimu ya ngono” ambayo inatambua mahusiano kabla ya ndoa, kama ni kawaida ya maisha, na pia upotovu mwingine. Haikubaliki kabisa kuruhusu programu kama hizo kwa wanafunzi. Shule imeundwa ili kupinga uovu unaoharibu uadilifu wa mtu binafsi, kuelimisha usafi wa kiroho, kuandaa vijana ili waweze kuunda familia zenye nguvu katika misingi ya uaminifu na usafi.

Tangu zama za kale, Kanisa limeweka msimamo kwamba ukatishaji wowote wa mchakato wa uzazi, wa kukusudia, (kutoa mimba) kuwa ni dhambi kubwa. Kanuni za Kanisa zinalinganisha utoaaji- mimba na uuaji. Tathmini hii inaegemea kwenye misingi kwamba kuzaliwa kwa mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu, na kwa hiyo, tangu muda wa kutungwa kwa mimba, ukatishaji wowote wa maisha ya mwanadamu-mtarajiwa huyu ni uhalifu.

Kanisa linachukulia kuenea na kuhalalishwa kwa utoaji-mimba katika jamii ya leo kuwa tishio kwa mustakabali wa ubinadamu na ni ishara ya wazi ya uharibifu wa maadili. Uaminifu kwa mafundisho ya kibiblia kuhusu utakatifu na thamani ya maisha ya mwanadamu tangu kuasiliwa kwake haiendani na kukubalika kwa dhana ya “uhuru wa kuchagua” ya mwanamke katika uainishaji wa hatima ya kijusi. Kanisa pia daima linaona kuwa ni wajibu wake kutetea wanadamu walio hatarini na walio tegemezi, ambao hawajazaliwa. Bila kuwatenga wanawake ambao wametoa mimba, Kanisa linawaita waje kutubu dhambi hiyo. Mapambano dhidi ya utoaji- mimba, ambayo wakati mwingine wanawake hulazimika kuuendea kutokana na uhitaji mkubwa wa kujikimu, pamoja na unyonge, yanalihitaji Kanisa na jamii kwa ujumla kuchukua hatua madhubuti za kulinda uzazi, na pia kuweka masharti ya kuasili watoto ambao mama, kwa sababu fulani-fulani, hawezi kuwalea peke yake.

Katika miongo ya hivi karibuni, nchi ambazo hapo awali zilijinasibu kuwa ni za Kikristo zimekuwa zikijaribu kuulazimisha ulimwengu mzima ufuate mfumo wa maadili yanayopingana, si tu na mafundisho ya injili, bali pia na maadili ya ulimwengu na hata akili ya kawaida. Hata hivyo, ni dhahiri kwa kila muumini kwamba kanuni za kimaadili zilizoamriwa na Mungu ni msingi usiotikisika wa maisha na maendeleo yenye kuleta mafanikio kwa kila mtu, binafsi na jamii kwa ujumla, na hazipaswi kusahihishwa ili kukidhi matakwa na hisia za mamlaka fulani za kisiasa. Uhifadhi na uthibitisho wa kanuni za maadili ya kitamaduni ndio ufunguo wa uwezekano na mustakabali wa ustaarabu mzima wa mwanadamu.

Kwa kutumia mifumo ya mwingiliano kati ya imani, kati ya dini na dini, serikali na kanisa-nchi, pamoja na kanisa-jamii na kutambua umuhimu wa kipekee wa ushuhuda wa pamoja katika mwelekeo huu, tunaitwa kutetea na kulinda maadili ya kitamaduni kwa njia-shirikishi, njia zote zilizopo na zinazokubalika kimaadili.

Kwa kumalizia, ningependa kutambua kwamba tangu kuanzishwa kwake, mnamo Desemba 2021, Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika imekuwa ikitunza vituo vya kulelea watoto yatima nchini Kenya: kituo cha Mtakatifu Petro Mtume kule Riga na cha Mtakatifu Atanasius Mkuu kule Nyabigega.

Wanalelewa na mapadri wetu – Padri Teodori Ouru na Padri Joji Otara. Kwa bahati mbaya, tulipokuja Afrika, tulikabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu ya kijamii na kiuchumi, hali duni ya maisha ya watu. Kwa mfano, katika makazi yaliyotajwa hakukuwa na maji ya bomba wala umeme. Kwa hivi sasa, tumerekebisha hali hii na hadi kufikia leo, tunafanya kila liwezekanalo, kutoa misaada, kujenga na kuboresha makazi, kuanzisha ufugaji wa kuku na wanyama, pia mashamba. Ila bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Nina hakika kwamba mawazo na malengo yaliyotolewa katika kongamano hili yatasikilizwa na jamii na yataainishwa katika sera za serikali, shughuli za elimu na kijamii, na pia katika ushirikiano wa karibu zaidi kati ya kanisa na serikali.

Ninawatakia msaada wa Mungu utiao nguvu, kazi njema yenye kuzaa matunda, mafanikio na dhamira kuu ya kulinda Utukufu wa Mungu.

Shirikisha katika mitandao ya kijamii:

Taarifa zote zilizo na maneno muhimu

-