Nafasi ya Dini katika Maendeleo ya Mataifa ya Afrika katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Nafasi ya Dini katika Maendeleo ya Mataifa ya Afrika katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi

Mnamo Julai 28, 2023, Katika jukwaa la Kongamano la Uchumi na Huduma za Kibinadamu la Urusi – Afrika, chini ya mwavuli wa Mkutano wa Kilele wa Pili wa Urusi – Afrika kule St Petersburg, kulifanyika kikao cha Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika kuhusu “Nafasi ya Dini katika Maendeleo ya mataifa ya Afrika katika ulimwengu unaobadilika kwa  kasi”.

 Askofu Mkuu wa Afrika, Metropolitani wa Klin Leonid alitoa hotuba kuu.

1. Dini ina nafasi kubwa zaidi katika bara la Afrika kuliko katika sehemu nyingine za dunia, kwa sababu, kwa ujumla Waafrika ndio watu wapenda- dini zaidi kuliko wengine wote duniani. Kuna idadi ndogo sana ya wasioamini, huku idadi ya waumini katika nchi nyingi za Kiafrika inakaribia asilimia mia moja (kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa kisosholojia uliochapishwa na gazeti la “The Telegraph” https://nonews.co/directory/lists /nchi/dini). Bado kuna umuhimu mkubwa wa dini na ushawishi wake katika michakato inayofanyika katika jamii, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kisiasa ya kijamii. Kwa hiyo, dini ndiyo inaweza kuwa msingi wa kuanzisha uhusiano wa muda mrefu na Afrika.

2. Waafrika wengi  ni wanaumini wa Ukristo. Kwa kuongezea, chaguo hili la kiitikadi lilifanywa na wawakilishi wa bara hili, kati ya wakazi wa kwanza kwenye sayari hii. Kristo mwenyewe aliizuru Misri, akiwa na Mama yake Maria, na kisha Mtume Marko akaanzisha Kanisa kubwa huko. Ethiopia ilikuwa moja kati ya nchi za kwanza kuuweka Ukristo katika ngazi ya kiserikali. Katika historia kuliluwa na Makanisa ya Afrika Kaskazini na Nubia yaliyotukuka na kuenziwa sana. Mapokeo yake yangali hai hadi leo na yanatuimarisha – wakristo wa sasa. Na kama tukizungumza juu ya Misri na Ethiopia, halafu tukaiongeza Eritrea huko, basi Makanisa halisi ya Kiafrika yangali yanashamiri huko hata hivi leo.

3. Jambo la kipekee lililochangia katika kuunda sura  ya dini katika Afrika ilikuwa ni ujio wa ukatoliki na uprotestanti – katika mfumo wa ukristo wa Kimagharibi, uliokuja ukiambatana na ukoloni. Baadaye, vikundi vingi vilijitokeza barani Afrika, ambavyo vilihama kutoka kwenye mfumo wa makanisa ya Magharibi na vikabuni mafundisho yao wenyewe, yakichanganya mafundisho ya Ukristo na mila zao za asili. Hii inaakisi shauku ya Waafrika kutafuta fursa za kukiri imani katika Kristo bila kuhusiana na Makanisa ambayo yamejichafua kwa kushiriki katika biashara ya utumwa, kuunga mkono wakoloni, pamoja na migogoro ya kikabila, kama vile, mauaji ya halaiki nchini Rwanda, na kwingineko barani. Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya waafrika kukatishwa tamaa na Makanisa ya Magharibi imeongezeka kutokana na mwenendo uliochukuliwa na Makanisa hayo kuasi mafundisho na maadili ya Biblia kwa kukumbatia dhana ya ushoga na usagaji, ujinsia, pamoja na nadharia ya usawa wa kijinsia.

4. Kutokea kwa Esarkia ya Afrika ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi kuliibua wimbi la shauku ndani ya mioyo ya watu wengi barani Afrika. Uothodoksi unakidhi matarajio mengi ya waafrika, hauna makwazo yaliyomo katika Makanisa ya Magharibi yaliyoelezwa hapo juu, na wakati huo huo ndilo Kanisa la asili la Kristo.

5. Kanisa la Kiohodoksi la Kigiriki la Aleksandria lina historia ya uwepo wa siku nyingi katika bara la Afrika, lakini kwa karibu muda wote limekuwa likizingatia kuhudumia raia wa Kigiriki tu wanaoishi katika nchi za Afrika. Ni katika karne ya ishirini tu ndipo ilipoanza kukua, kwa kiasi fulani, kutokana na kuanza kupokea vikundi vya waafrika  vilivyoamua kujihusisha na Uothodoksi. Lakini, pamoja na mafanikio hayo, kwa ujumla, Kanisa la Aleksandria bado halikuweza kukidhi kiu na matarajio ya waafrika na lilizidi kuwakatisha tamaa wengi wao, kwani lilijikita zaidi katika kupandikiza itikadi inayoitwa Uyunani, bila kujali wala kuzingatia utambulisho na tamaduni wa Kiafrika.

6. Kanisa la Kiothodoksi la Urusi lina historia ndefu ya kuwepo barani Afrika. Kama alivyosema Mtakatifu Patriarki jana,katika hotuba yake, makanisa ya muda, ya Kirusi, yalianzishwa  kule Abyssinia katika karne ya 19, na mnamo mwaka wa 1914 parokia ya kudumu ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi ilianzishwa nchini Misri, na katika miaka ya 1920 – parokia za Kirusi zilianzishwa pia Tunisia, Algeria na Moroko. Tangu katikati ya karne ya ishirini, Kanisa letu lilijaribu kupanua uwepo wake barani Afrika kwa kushirikiana na Kanisa la Kiothodoksi la Aleksandria, jambo ambalo halikuwezekana, hasa baada ya Patriarki wa Aleksandria, akiwa chini ya shinikizo kutoka kwa mataifa hasimu wa Urusi, kuutambua  uasi na mpasuko wa Ukraina na kisha kuamua kuunda ushirika nao.

7. Tukio la kipekee na la kihistoria linashuhudiwa hivi sasa  – ukuaji wa kasi wa ufuasi wa Uothodoksi wa Kirusi katika “Bara  Jeusi”. Ndani ya mwaka mmoja na nusu tu wa uwepo wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika, idadi ya parokia za Kanisa la KIothodoksi la Urusi imeongezeka kutoka tano hadi mia mbili, na idadi ya nchi ambazo parokia hizi zimo, imeongezeka kutoka nne hadi ishirini na tano. Idadi kubwa ya mapadri na waumini wa kanisa hilo ni Waafrika. Hakika Kanisa la Kiothodoksi la Urusi  ndilo linaloweza kuwa, na tayari ni daraja linalounganisha nchi na watu wetu na kufunua undani wa kila mmoja wetu. Wakati huo huo, taratibu zinazojulikana kama ugeuzaji- imani na upanuzi, ni ngeni kwa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi. Linafungua milango kwa kila mtu anayetamani upya wa kiroho ndani ya mfumo, mila na taratibu za ukristo wa Kiothodoksi. Pia liko tayari kushirikiana na madhehebu mengine na jumuiya za kidini. Tuna ajenda pana ya ushirikiano – ulinzi wa misingi ya asili ya maisha ya binadamu, maadili, madai ya uhuru wa kuabudu, kupigania amani, huduma za kibinadamu. Tayari tunashirikiana kikamilifu na Makanisa ya Kikoptiki na Ethiopia, mashirika ya Kiislamu, na jumuiya za Kikatoliki na Kiprotestanti, na mabaraza ya kidini na ya mashirikiano kati ya Waumini wa kikristo katika nchi mbalimbali. Tuna hakika kwamba uzoefu ambao tumeupata katika mwingiliano wa kidini kati yetu na Waislamu pamoja na wawakilishi wa dini zingine nchini Urusi, na nchi zingine zilizo chini ya dhamana yetu ya kikanuni, pia utatufaa katika huduma yetu, na ninamkaribisha mtukufu Mufti Albir Krganov, mkuu wa Baraza la Kiroho la Waislamu. wa Urusi, ambaye pia yuko hapa, kuzungumza juu ya haya yote.

8. Yafaa kutambua kwamba maisha ya kisiasa ya Afrika si shwari. Kuna migogoro, na ili kuikoleza, mara nyingi hujaribu kutumia sababu za kidini. Kwa bahati mbaya, Wakristo wanateswa katika nchi kadhaa za Afrika. Amani ni kitu ambacho nchi nyingi na watu wanakihitaji sana hivi leo, hususan pamoja na bara la Afrika, na Kanisa la Kiothodoksi la Kirusi linakuja Afrika na ujumbe wa amani, ujirani mwema na maelewano.

Askofu Mkuu wa Esarkia ya Afrika

Shirikisha katika mitandao ya kijamii: