Salamu za Pasaka za Metropolitani wa Klin Leonid kwa Makasisi, Watawa na Walei wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika na Dayosisi ya Yerevan-Armenia - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Salamu za Pasaka za Metropolitani wa Klin Leonid kwa Makasisi, Watawa na Walei wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika na Dayosisi ya Yerevan-Armenia

Askofu Mkuu Metropolitani wa Klin Leonid alituma salamu za Pasaka kwa makasisi, watawa na walei wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika na Dayosisi ya Yerevan-Armenia.

KRISTO  AMEFUFUKA!

Wapendwa akina baba, kaka na dada zangu katika Bwana!

Kwa moyo wa upendo ninawapongezeni katika sikukuu tukufu ya Pasaka ya Bwana!

Kristo, baada ya Kufufuka Kwake ile siku ya tatu, alionekana mara kadhaa kwa mitume watakatifu na wanawake waliobeba manemane ili waweze kusadiki kwamba kweli amefufuka kutoka kwa wafu. Lakini siyo papo hapo, na si kila mtu aliamini, kwani tukio hili lilikuwa la kushangaza sana na kimsingi lilipingana na uzoefu na hata mantiki ya maisha ya mwanadamu. Zaidi ya hayo, muonekano wa Mwokozi, baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu, ulikuwa umebadilika sana kiasi kwamba wengi hawakuweza kumtambua. Roho Mtakatifu tu ndiye aliyeshuka juu ya mitume siku ya Pentekoste, akawaimarisha katika imani yao katika Ufufuo wa Kristo na kuwapa nguvu ya kuibeba imani hii, ambayo sasa haina shaka wala wasiwasi wowote, kwenda ulimwenguni na kuwafahamisha  wanadamu.

Siri ya Ukristo ni kwamba tunakuja kwa Kristo kabla hatujamwona, kwa sababu tunaanza kuamini. Katika Injili tunasikia maneno ya uzima na taratibu maono ya Bwana Mfufuka yanafunuliwa mbele yetu. Tunasonga kutoka imani isiyo na  ufahamu hadi imani yenye mantiki wakati Mwokozi anajifunua kwetu.

Haiwezekani kuja kwa Ukristo isipokuwa kwa kumpenda Bwana Yesu, Aliyekufa na kufufuka tena. Haiwezekani kuwa Mkristo kwa hisia tu za mafundisho ya maadili ya Kristo au kwa kuheshimu  tu neno Lake. Bali, baada ya  kumpenda Mwana wa Mungu, mtu anaweza kuifikia imani ambayo haiwezi kuelezeka kwa maneno, kwa sababu iko juu ya maono ya kawaida ya kidunia. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Kristo akitoka kaburini, lakini ndani ya kila mmoja wetu kuna uhakika kwamba alifufuka kweli. Ujasiri huu unaimarishwa kila wakati tunaposhiriki Mafumbo Matakatifu, tunamgundua tena Mwokozi Mfufuka ndani yetu hasa Yule ambaye awali aliwatokea wanafunzi wake.

Mwinjilisti Luka anatuambia kwamba wasafiri waliokuwa wanakwenda Emau hawakumtambua Kristo, ila kadri walivyokwenda naye zaidi, ndivyo walivyohisi kitu fulani ambacho wanakifahamu sana juu Yake jambo ambalo walilijua kutokana na uzoefu wa kuwa Naye. Huu ndio ujasiri tunaoupata kupitia tukio la Ufufuo, wakati, tunapokufa pamoja na Mwokozi katika Wiki Takatifu, tunafufuka pamoja naye katika usiku wa Pasaka.

Ufahamu  juu ya Bwana Mfufuka  unatolewa kwetu kwa namna ya kipekee kabisa katika siku hizi za Pasaka. Ni lazima tuwe wastahili wa tukio hili, tuwe kama vile wanafunzi wake walivyokuwa baada ya Kristo kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu” (Yoh 20:22). Wao, waliokuwa wamemwona Yesu hapo awali, lakini hawakumtambua Mungu Mwenye Mwili ndani Yake, sasa waliweza kusema:” Tumeuona Ufufuo wa Kristo.”                                 

Pia tunafundishwa kuhusu Roho Mtakatifu kupitia Sakramenti za kanisa. Kwa hivyo, kila mmoja wetu ana wajibu na utume ambao mitume walikabidhiwa – kumhubiri Kristo. Tukio la Pasaka halijatolewa ili kwamba, baada ya kufurahia ukaribu wa Mwokozi Mfufuka, tuifiche nuru yake katika hazina yetu ya ndani, bali ili tuipeleke furaha hii kwa wote walio karibu na pia walio mbali – kwa ulimwengu ambao Bwana anataka kuuangaza kupitia sisi kwa Ufufuo wake.

Mchanganyiko wa shaka na imani umewatesa wakristo kwa karne nyingi: wapo waliomwabudu Kristo kama Mungu na Mwokozi, wakati wengine waliutilia shaka ukweli wa Ufufuo. Wengine walijenga Kanisa la Mwenyezi Mungu, wakatoa maisha yao kwa ajili ya Injili, ila wengine walibuni mafundisho yao wenyewe, wakarudi nyuma na kujiingiza katika uasi au madhehebu-potofu kwa sababu waliutilia shaka Ufufuo wa Kristo na ukweli kwamba Yeye ndiye Mungu. Majaribio kama hayo yamekuwapo na yataendelea kuwapo, ila sisi tunaomwamini Masihi Yesu, tunajua kwamba Yeye ndiye Bwana wetu, Aliyefufuka siku ya tatu. Tunajua kuhusu hili kwa sababu historia nzima ya Kanisa na uzoefu wetu sisi wenyewe, wa maisha ndani yake, huthibitisha kwamba Kristo hakika alifufuka kwa sababu yeye ni Mungu mwenye mwili, na ili kufungua njia ya ufufuo kwa watu wote.

Katika siku hizi za Pasaka tunaaswa tena kufikiria juu ya mantiki ya kuwepo kwetu hapa duniani kama ni muda tuliopewa ili tujiandae kwa umilele na tayari, katika ulimwengu huu, tuweze kumwona Mwokozi Mfufuka kwa macho ya kiroho, kama Mtume Tomaso, akiwa ameweka kando mashaka yote, alimkiri Yeye kwa maneno: “Bwana wangu na Mungu wangu!” ( Yoh 20:28 ) – kwa moyo na roho yake yote.

Ninawapongezeni waumini wote wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi wanaoishi katika bara la Afrika na katika Jamhuri ya Armenia katika Sikukuu ya Ufufuo Ung’aao wa Kristo, ninawaombea kwa Mwokozi Mfufuka furaha ya kiroho, mafanikio katika imani na ucha-Mungu, msaada, neema na baraka za Mungu katika kazi zenu, afya njema, amani na maisha marefu!

KRISTO  AMEFUFUKA   KWELI!

+LEONID, Metropolitani wa Klin, Askofu Mkuu wa Esarkia ya Afrika

Pasaka ya Kristo

Ya 2023

Shirikisha katika mitandao ya kijamii:

Taarifa zote zilizo na maneno muhimu