Ujumbe wa Krismasi wa Patriarka Kirill wa Mosko na Urusi Yote - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Ujumbe wa Krismasi wa Patriarka Kirill wa Mosko na Urusi Yote

Ujumbe wa Krismasi

wa

Patriarka Kirill wa Mosko na Urusi Yote

kwa  wachungaji-wakuu, wachungaji, mashemasi,watawa

na  waumini  wote  wa  Kanisa la Kiothodoksi  la Urusi

Wachungaji-wakuu  wapendwa wa Bwana, Waheshimiwa  Makasisi na  Mashemasi,  Watawa  wapenda-Mungu,  wapendwa  kaka  na  dada  zangu!

Hivi sasa, wakati Kanisa la Mbinguni na Duniani linapomtukuza Mungu aliyetwaa mwili katika umoja wa upatanisho, ninawapongeza ninyi nyote kwa moyo mkunjufu kwa sikukuu  inayong’aa ya Kuzaliwa kwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Leo tunarejesha kumbukumbu zetu kwenye matukio yaliyojili zaidi ya miaka elfu mbili ziliyopita kule Bethlehemu. Tunamtazama Mtoto mpole akiwa amelala horini amezungukwa na Mama-asiye na doa, Yusufu-mwadilifu na wachungaji, ambao habari za kuja kwa Mwokozi duniani ziliwasilishwa kwao kwanza, na tunarejelea Mwangwi wa Majeshi yasiyo na Mwili yanayomtukuza Muumba Mkuu kupitia Mwanawe wa Pekee ambaye alileta amani na mapenzi mema kwa wanadamu.

Mtakatifu Gregori, Mtheolojia, akifafanua kiini cha sikukuu hii, alishuhudia: kwamba ushindi wetu ni juu ya kuja kwa Mungu kwetu wanadamu, ili tuweze kurudi kwa Mungu (Neno 38). Sasa Ufalme wa Mbinguni umetukaribia kweli kweli ( Mt. 3: 2 ): katika kutimilika kwa unabii wa kale, Mpatanishi aliyengojewa kwa muda mrefu sasa amekuja duniani ( Mwa. 49: 10 ), Mtoto amezaliwa kwetu— tumepewa Mwana; na jina lake ni: Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani (Isa. 9: 6).

 Amani yangu nawapa; niwapavyo mimi si kama ulimwengu utoavyo (Yohana 14:27), – Kristo anatuhutubia. Je! ni amani ya aina gani hii ambayo Bwana alimpa mwanadamu na ambayo malaika waliiimba wakati wa kuzaliwa kwa Mwokozi? Je, kumekuwa na kupungua kwa uadui au migogoro duniani kuanzia wakati huo? Tunasikia "amani, amani!" kutoka kila pembe ya nchi, lakini bado hakuna amani, kulingana na neno la nabii (Yer. 8: 11). Lakini amani ya kweli ya Mungu, ambayo ilishuka duniani pamoja na Kuzaliwa kwa Kristo, ni zaidi ya akili yoyote (Flp. 4:7). Yeye hategemei hali ya nje na hayuko chini ya huzuni na ugumu wa maisha ya muda. Amani hii ya ndani isiozuilika, imo ndani ya Mungu Mwenyewe, ambaye, akiwa amefanyika mwanadamu, katika kila kitu kama sisi, isipokuwa dhambi, haifanyi kazi katika historia yetu tu, lakini iko wazi ndani yake. Sasa Neno amefanyika mwili, akakaa nasi, amejaa neema na kweli (Yohana 1:14). Bwana yu karibu, wapendwa wangu - tusisahau kamwe juu yake na tusife moyo!       Ndani yake mna nguvu zetu, tumaini letu lenye nguvu na faraja ya kiroho katika hali zote za maisha.
Huku tukisujudia ukuu mnyenyekevu wa muujiza wa ufanyikaji-mwili wa Mungu na kumtukuza Mwokozi aliyekuja ulimwenguni hatuwezi wakati huo huo, kutokuwa na wasiwasi juu ya matukio ya kijeshi yanayojili hivi sasa, yakiifunika sherehe takatifu ya Krismasi, kwa sababu kama mtume anavyobainisha, kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote vingine huumia pamoja nacho (1 Kor. 12: 26). Katika majaribu haya ambayo yamewapata watu wa Urusi ya kihistoria, ni muhimu sana kwetu kuthibitisha uaminifu wa wito wetu wa Kikristo na kuonyesha upendo kwa kila mmoja. Wakati mwingine inaonekana kuwa wema na upole ni udhaifu na kwamba hauna utetezi, na kwa kiasi fulani unategemea juhudi zetu ndogo. Hata hivyo, hali haiko hivyo.
Kuna kanuni ya kiroho isiyobadilika: upendo huongezeka tunapojitoa kwa wengine, tunapotoa wakati wetu kwa jirani zetu, kusaidia kwa vitu au hata tu kuwaonyesha kuwa tunawajali. Kisha sisi sio tu hubadilisha ulimwengu unaotuzunguka, bali pia tunapata kitu cha thamani sana ndani yetu. Katika kanuni hii nyepesi, lakini yenye ufanisi wa kiroho, iko siri ya amani na furaha ya kweli, ambayo kila mtu anatamani sana kuipata. Furaha hii haiko mbali, kama baadhi ya watu wanavyoamini, wakivutwa na ushawishi wa mali na maisha ya kutojali. Furaha ya kweli ni kushiriki upendo na furaha pamoja na wengine, na kumtukuza Mungu kwa matendo mema, Yeye aliyefanyika mwili ili tuwe na uzima na tuwe nao tele (Yohana 10:10). Tunapomkaribisha Kristo katika mioyo yetu na kumruhusu afanye kazi ndani yetu, amani iliyobarikiwa pamoja na utulivu hutawala ndani ya roho zetu (Mathayo 11:29), na tunakuwa washiriki wa Ufalme wa Mungu ulio ndani yetu (Luka 17:21).
Je, tunataka kumkumbatia Bwana aliyezaliwa? Basi na tuwakumbatie wanaohuzunika na tuwafariji wanaoteseka. Je, tunataka kumgusa Kristo na, kama wahenga wa Mashariki- kuleta zawadi za kupendeza kwa Mtoto-Mungu? Basi na tutoe upendo na matunzo kwa wapendwa wetu, tuwapatie wahitaji huruma, rehema na tuwasaidie waliovunjika moyo. “Kama mlivyomtendea mmoja wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mathayo 25:40), Mwokozi anashuhudia.
"Usiku wa Krismasi huleta amani na utulivu kwa ulimwengu!" anatamka Mtawa Efraimu Mshami na anaendelea kwa ujasiri: "Usiku huu ni wa Wanyenyekevu, basi kila mtu na aweke kando ghadhabu na ubaya. Sasa siku ya rehema imepambazuka, ili kwamba kusiwe na mtu anayefuatilia kosa alilotendwa kwa kulipiza kisasi. Siku ya furaha imefika ili mtu yeyote asiwe sababu ya huzuni au huzuni kwa mwingine" (Nyimbo za Krismas: I).
Hebu na tusikilize maneno haya ya kustaajabisha ya “Nabii Mshami wa jangwani” na tufungue mioyo yetu kwa Bwana aliyefanyika mwili kwa ajili yetu. Na tushangilie, kwa maana Mfalme na Mtawala wa ulimwengu wote, Yeye Mwenyewe amekuja duniani kwa upole na unyenyekevu ili kutupatia wokovu na uzima wa milele. Na sisi, huku tukiitikia kwa shukrani na upendo mkuu wa Muumba kwa watu, tutakase nafsi zetu kwa kuvumilia majaribu kwa subira, kwa sala changamfu na kwa matendo mema, kwa utukufu wa Mungu.
Kwa mara nyingine tena ninawapongeza ninyi nyote wapendwa wangu, kwa sikukuu ng’avu ya Kuzaliwa kwa Kristo, ninawatakia furaha isiyo na ukomo na ustawi katika nyumba na familia zenu, nguvu na msaada-karimu  kutoka kwa Bikira-mbarikiwa Yesu. Muumba mwenye utu, Bwana wa kweli wa Historia, na ashushe huruma yake kwa watu wa Urusi takatifu na atubariki sisi sote kwa amani, ili kwa kinywa kimoja na moyo mmoja tumtukuze Mwokozi aliyefanyika mwili na tushuhudie kwa hakika kwamba Mungu yu pamoja nasi!
PATRIARKA  WA MOSKO NA URUSI ZOTE
Krismasi 2022/2023
Mosko
Shirikisha katika mitandao ya kijamii:

Taarifa zote zilizo na maneno muhimu