Kasisi kutoka Afrika awaeleza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theolojia cha St. Petersburg kuhusu taratibu za liturgia za Wakristo wa Kiothodoksi nchini Tanzania - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Kasisi kutoka Afrika awaeleza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theolojia cha St. Petersburg kuhusu taratibu za liturgia za Wakristo wa Kiothodoksi nchini Tanzania

Mnamo Septemba 19, 2023, Chuo Kikuu cha Theolojia cha St. Petersburg kilifanya mhadhara wa kwanza katika kuzindua mwaka mpya wa masomo, kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa masomo ya Liturgia.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Padri wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika kutoka Tanzania, mwanafunzi katika kitivo cha theolojia na uchungaji, Kasisi Mkuu Zacharia (Mulingwa), na ambaye  alitoa mhadhara juu ya mada “Ibada ya Kiothodoksi nchini Tanzania”.

Padri Zakaria alieleza kuhusu historia ya maendeleo ya Kanisa la Kiothodoksi nchini Tanzania. Ili  kufafanua zaidii, mhadhiri alitumia picha na video zinazoonyesha hali ya Kanisa katika bara la Afrika.

“Kuna wakristo wa Kiothodoksi wapatao elfu 700 nchini Tanzania, na kuna makabila 121, ambapo kila moja lina lugha yake, utamaduni na ngoma zake. Lakini makabila na lugha zote zinaunda utamaduni mmoja – wa Kiswahili. Katika kutoa huduma ya umisionari ni lazima kuzingatia tofauti za kitamaduni kati ya makabila,” Padri Zakaria alibainisha katika utangulizi wa taarifa yake hiyo.

Washiriki wa mhadhara huo walifurahishwa sana na video iliyowaonyesha waumini wa Kitanzania wakicheza ngoma baada ya Liturgia. Padri Zakaria alifafanua kwamba hairuhusiwi kucheza ngoma wakati wa ibada hekaluni, na kwamba kwa kawaida shamrashamra hizi hufanyika nje – baada ya ibada.

Na wakati mwingine, mra moja moja, hii hufanyika wakati wa huduma endapo ibada inafanyika nje – kivulini: “Hatuna utamaduni kama kule Urusi wa kula au kunywa chai baada ya ibada. Huwa tunatoka tu nje na kushereheka. Sehemu kubwa ya uinjilishaji, hasa nchini Tanzania, hufanywa kwa njia ya uimbaji na kucheza muziki.” Baada ya mhadhara huo Padri Zakaria alijibu maswali ya wasikilizaji wake.

***

Mikaeli Rizhov, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Uzamili: Nani huandika nyimbo za Kikristo nchini Tanzania

— Tuna watu tofauti-tofauti wanaoandika nyimbo hizo. Mara nyingi huchukua maandiko kutoka kwenye zaburi na kuyarekebisha kidogo ili kuendana na utamaduni wa muziki wa nchi-husika. Wakati mwingine huchukua maandiko kutoka kwenye masomo ya Jumapili.

— KasisiMtawa Gennadi (Polyakov): Je, unapendelea zaidi wanapokuwa wameketi wakati wa ibada au wanapokuwa wamesimama?

— Nchini Tanzania, kabla ya Ukristo, kulikuwa na imani za asili, ambazo kwa kawaida watu walikwenda mahali fulani – maalum, pa ibada yao, na kusimama pale – kwa utii. Hivyo tunapendelea kila mtu asimame ili kwamba isionekane kuwa kuabudu ni rahisi tu. Tunajaribu kurejea kwenye mila ambazo  kila mtu alisimama. Sasa, tunapoomba, tunasimama. Baada ya ujio wa ukoloni, mila ya kukaa wakati wa ibada ilijitokeza. Kwangu mimi binafsi, ni makosa kuketi wakati wa huduma takatifu. Ni bora kusimama na kusujudu, kwa sababu kuutafuta uso wa Mungu si kazi rahisi.

***

Baada ya kipindi hicho cha maswali na majibu, muongoza – mhadhara, Makamu Mkuu wa Chuo kwa Masuala ya Taaluma, wa Chuo hicho, Kasisi Mkuu Vladimir Hulap, alimshukuru na kumpongeza Kasisi Mkuu Zakaria kwa kupata fursa ya kujifunza zaidi mapokeo ya kiliturgia ya Kanisa la Kiothodoksi nchiniTanzania. Baba Vladimir alionyesha matumaini ya muendelezo wa mawasiliano na ushirikiano wa karibu zaidi katika shughuli na miradi ya pamoja.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa sala ya pamoja ya “Baba Yetu …..”, ambayo wanafunzi wa Kiafrika waliifanya kwa lugha ya Kiswahili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanafunzi pamoja na waalimu wa Shule ya Theolojia ya Mji Mkuu, na pia taasisi zingine za theolojia, za Kanisa la Kiothodoksi la Urusi. Mazungumzo hayo yalifanyika kwa Kiingereza na kutafsiriwa kwenda lugha ya Kirusi na mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya kwanza – Vitali Demin.

 

Shirikisha katika mitandao ya kijamii:

Taarifa zote zilizo na maneno muhimu

-