Katika mkutano wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, uliofanyika Desemba 29 , washiriki walijadili azimio la Sinodi ya Patriarkia ya Aleksandria kuhusu “kushushwa cheo” kwa Askofu Mkuu wa Afrika, Metropolitani wa Klin Leonid.
JARIDA Na. 136
WATOA HOJA ; juu ya azimio la Sinodi ya Patriarkia ya Aleksandria kuhusu “kushushwa cheo” kwa Askofu Mkuu wa Afrika, Metropolitani wa Klin Leonid.
Hoja:
Kuhusiana na kutambuliwa rasmi kwa kanisa linalojiita Kanisa la Kiothodoksi la Ukraina na Patriaki Theodore wa Aleksandria tarehe 8 Novemba, 2019, na kisha yeye kumuadhimisha mkuu wa muundo huu usio wa kikanuni, katika liturgia, Sinodi Takatifu, katika mkutano wake wa tarehe 26 Desemba, 2019 ilithibitisha “kutokuwepo tena kwa uwezekano wa kuadhimisha jina la Patriarki Theodore wa Aleksandria katika diptiki, na pia kuwa na ushirika naye katika maombi na Ekaristi“ na ikasitisha mawasiliano ya kikanisa na maaskofu wa Kanisa la Kiothodoksi la Aleksandria, ambao “waliunga mkono au katika siku zijazo wataunga mkono uhalalishwaji wa uasi na mgawanyiko katika Kanisa la Ukraina” (jarida Na. 151).
Baadaye, Patriarka Theodore wa Aleksandria , si tu hakupinga kumwadhimisha mkuu wa kikundi kilichotajwa hapo juu, bali pia alihudumu naye katika liturgia kwenye kisiwa cha Imvros tarehe 13 Agosti, 2021. Akijibu maombi mengi kutoka kwa makasisi wa Patriarkia ya Aleksandria, ambao hawakutaka kuwa washiriki katika matendo ya kuvunja kanuni , yaliyotekelezwa na Patriarki wao, na wakaomba wakubaliwe kuwa chini ya mamlaka ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, na kwa kuzingatia ukweli kwamba Patriarki Theodore ndiye aliyefungua njia ya mgawanyiko huo, Sinodi Takatifu, katika mkutano wake wa tarehe 29 Desemba, 2021(jarida Na. 100) iliamua kuunda Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika) na kumteua Metropolitani wa Klin Leonid kuwa mkuu wake.
Sinodi Takatifu, katika taarifa yake ya Januari 28, 2022, ilibainisha kwamba uamuzi juu ya kuundwa kwa esarkia, "uliopitishwa huku kukiwa na mazingira ya kutambuliwa kwa waasi wa Ukraina na Patriarki wa Aleksandria, kwa namna yoyote ile kusichukuliwe kuwa ni kauli ya madai ya kupokonya eneo la kikanuni la Kanisa la kale la Aleksandria, bali unaofuata lengo pekee – la kutoa ulinzi wa kikanuni kwa wale makasisi wa Kiothodoksi barani Afrika, ambao hawataki kuwa washiriki katika uhalalishaji wa uasi na mgawanyiko nchini Ukraina."
Barua za Patriarki Theodore wa Aleksandria, za Januari 12 na Februari 14, 2022, zilizotumwa kwa Patriarki wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi zilikuwa na tishio la "kushushwa cheo" kwa Metropolitani wa Klin Leonid. Patriarki wa Mosko na Urusi Yote Kirill alituma jibu kwa jumbe mbili (barua za Januari 18 na Machi 5, 2022). Katika barua yake ya mwisho, Mwadhama Patriarki, kipekee alimwambia Patriarki Theodore, "kwamba maamuzi yoyote ya kimahakama ya Kanisa lako kuhusu Metropolitani wa Klin Leonid au maaskofu wengine au makasisi wa Kanisa letu, yatatambuliwa nasi kuwa hayana nguvu ya kikanuni na ni batili."
Mnamo tarehe 22 Novemba, 2022, Sinodi Takatifu ya Patriarkia ya Aleksandria ilipitisha azimio "kuhusu kushushwa cheo kwa Metropolitani wa Klin Leonid."
WAAZIMIA:
Katika kutilia maanani kuegemea kwa Patriarki Theodore wa Patriarkia ya Aleksandria kwenye mpasuko (kutambua kwake uasi wa kikundi cha watu ambao hawana neema ya ukuhani, na waliotengwa na Kanisa, na kuwa na ushirika wa Ekaristi nao, kuunga mkono mgawanyiko ndani ya Kanisa la Kiothodoksi la Ukraina), na kwa kuzingatia kanuni, mila na taratibu zinazotambulika kwa ujumla, za kwamba Kanisa moja linalojitawala lenyewe halina mamlaka ya kimahakama dhidi ya Kanisa lingine ambalo nalo linajitawala lenyewe, azimio la Sinodi ya Patriarkia ya Aleksandria kuhusu "kushushwa cheo" kwa Askofu Mkuu wa Afrika, Metropolitani wa Klin Leonid, na maamuzi mengine yote yanayofanana na hayo, kuhusu makasisi wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, kuwa hayana nguvu ya kikanuni na ni batili.