Ujumbe wa Kanisa la Ethiopia wazuru Urusi - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

Ujumbe wa Kanisa la Ethiopia wazuru Urusi

Mnamo Februari 11, 2023, kwa mwaliko wa Mtakatifu Patriarki wa Mosko na Urusi Yote Kirill, na kwa baraka za  Mtakatifu Patriarki-Katholikos wa Ethiopia Abuna Matayo, wajumbe wa Kanisa la Ethiopia waliwasili Mosko ili kushiriki katika kikao cha pili cha Tume  ya Majadiliano kati ya Kanisa la  Kiothodoksi la Urusi na Kanisa la Ethiopia.

Ujumbe uliowasili uliundwa na: Askofu Mkuu wa 

Omo Kusini Abuna Filipos, Mkuu wa Chuo cha Theolojia cha Utatu Mtakatifu kilichoko Addis Ababa, Mwenyekiti-Mwenza wa Tume Padri Daniel Seifemihael, Mkuu wa Idara ya Mahusiano na Nje ya Kanisa la Ethiopia, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Patriarkia ya Ethiopia, Katibu wa Tume;  Padri Weldeius Sefugalato, Naibu Mkurugenzi wa Masuala ya Kanisa la Ethiopia, Msimamizi wa parokia za Addis- Ababa.

Kwa upande wa Patriarkia ya Mosko, kikao hiki kinahudhuriwa na: Metropolitani wa Klin Leonid, Askofu Mkuu wa Esarkia ya Kipatriarki  ya Afrika, Mwenyekiti - Mwenza wa Tume; Shemasi Mtawa Stefan (Igumnov), Katibu wa Idara ya Mawasiliano na Nje ya Patriarkia ya Mosko kwa Mahusiano kati ya Wakristo, Katibu wa Tume; V.V. Kipshidze, Naibu Mwenyekiti wa Idara ya Sinodi ya Mahusiano ya Kanisa  na Jamii pamoja na Vyombo vya Habari; Shemasi Dimitri Serov, Mkurugenzi wa Idara  ya Uchapishaji ya Chuo Kikuu  cha Theolojia cha Mosko; S.G. Alferov, mfanyakazi wa Idara ya Mawasiliano na Nje  (IMN) ya Kanisa.
Walipofika Mosko, wajumbe wa Ethiopia walitembelea Makazi ya watawa ya Pokrovski Stavropol, ambapo watakaa kwa muda wote watapokuwa  wageni wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi.
Siku hiyo hiyo, mkutano ulianza. Akifungua mkutano wa Tume hiyo, Metropolitani wa Klin Leonid aliwaomba wajumbe kutoka Addis Ababa kufikisha  salamu za mshikamano na kusaidiana kutoka kwa Mtakatifu Patriarki Kirill kwa Askofu Mkuu, Sinodi na waumini wote wa Kanisa la Ethiopia, ambalo leo linapita katika nyakati ngumu ​​kutokana na majaribio ya kikundi cha waasi kutaka kusababisha mpasuko wa kanisa.
"Tunafurahi sana leo kuwakaribisheni hapa Mosko. Nchi yenu inapitia wakati wa wasiwasi tena. Hapana shaka kwamba matukio ya kutisha yanayojili nchini Ethiopia si ya bahati mbaya bali ni sehemu tu ya mnyororo mrefu wa mashambulizi yanayochochewa. Kwa sasa, Ethiopia na karibu nchi zote za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zinakabiliwa na tishio kubwa.Wakati huo huo, shinikizo kubwa zaidi linaelekezwa kwa serikali ya Urusi na kwa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi. Wanajaribu kuleta uharibifu na dhiki kubwa,  kwa kadri iwezekanavyo, kwa watu wetu. Nasi  tunahitajika  kukabiliana na changamoto hizi kwa umoja na pamoja  zaidi sasa kuliko  wakati mwingine wowote," Baba Leonid alibainisha.
Katika majibu yake, Askofu Mkuu Abuna Filipos, kwa niaba ya Patriarki Abuna Matayo, alishukuru sana kwa hatua zilizochukuliwa na Kanisa la Kiothodoksi la Urusi katika kuwasaidia Wakristo wa Ethiopia, ikiwa ni pamoja na barua za kuliunga mkono Kanisa la Ethiopia, zilizotumwa hivi karibuni na Mtakatifu Patriarki Kirill na pia  Mwenyekiti wa IMN  Metropolitani  wa Volokolamski Anthoni.
"Leo tuna wakati mgumu sana, vikosi vya kutisha vimeshika silaha na kujipanga dhidi yetu. Lakini watu wetu, muda wote, wamekuwa wakifikiwa na msaada wa kindugu wa Kanisa kuu la Kiothodoksi la Urusi. Na sasa tunamshukuru sana Mungu kwa kutupatia fursa ya kuendelea kuishiriki furaha. ya umoja na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya utukufu Wake katika nyakati hizi zinazovuma kama mawimbi,” Askofu Mkuu Filipos alisema.
Katika ratiba ya ziara ya ujumbe wa Kanisa la Ethiopia mjini Mosko, ambayo itaendelea hadi Februari 16, kumepangwa  mkutano na Mtakatifu Patriarki Kirill, ziara za kutembelea taasisi za sinodi, taasisi za elimu za Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, makanisa na makazi ya watawa  yaliyopo jijini Mosko na katika mkoa wa Mosko.
                                                              ***
 
Kanisa la Ethiopia ni sehemu ya familia ya Makanisa ya Kale ya Mashariki na si tu kwamba ni kubwa zaidi kati ya Makanisa ya mapokeo ya nyakati za kabla ya Ukalkedoni, bali pia ni moja ya Jumuiya  za Kikristo zenye watu wengi zaidi ulimwenguni: idadi ya waumini wake inazidi watu milioni 60.
 
Uhusiano kati ya watu wa Urusi na Ethiopia ulianza karne ya XV. Mawasiliano ya mara kwa mara kati ya makanisa yalianzishwa mwishoni mwa karne ya XIX. Mnamo miaka ya 1950-1980, yalifikia kiwango cha juu sana, kwa kiasi fulani ni kutokana na juhudi za Metropolitani wa Leningrad na Novgorod Nikodim, Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya Kanisa na Nje ya Patriarkia ya Mosko. Na leo yanaungwa mkono zaidi, ikiwa ni pamoja na  muundo wa ndani  wa shughuli za Tume ya Majadiliano kati ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi na Kanisa la Ethiopia.
Makubaliano ya uundaji wa Tume yalifikiwa na  Mtakatifu Patriarki Kirill na Mtakatifu Patriarki Matayo wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Kanisa la Ethiopia nchini Urusi mnamo Mei 15-20, 2018. Mapema, mnamo Novemba 2017 na Machi 2018, mikutano ya kikosi-kazi kwa ajili ya  kutayarisha mazungumzo, ilifanyika katika miji ya Mosko na Addis Ababa . Mnamo Julai 14, 2018, muundo wa Tume uliidhinishwa na Sinodi Takatifu ya Kanisa la  Kiothodoksi la Urusi, na mnamo Desemba mwaka huo huo, Sinodi ya Kanisa la Ethiopia ilipitisha azimio kama hilo. Mkutano wa kwanza wa Tume ulifanyika Januari 21-25, 2019 katika mji mkuu wa Ethiopia.
Maeneo muhimu ya ushirikiano baina ya pande hizi mbili ni: kukabiliana na chuki dhidi ya Ukristo; kulinda maadili ya asili katika ulimwengu wa leo; kusaidiana katika huduma za kichungaji kwa waumini wa Makanisa haya mawili, wanaoishi nchini Urusi na Ethiopia; uratibu wa mwingiliano kati ya Makanisa haya mawili katika ngazi ya jumuiya za kigeni na majukwaa ya kimataifa; mahusiano katika nyanja za elimu na makuzi ya vijana; ushirikiano katika uwanja wa sanaa ya kanisa na  uzalishaji wa vyombo vya kanisa; kubadilishana uzoefu katika majukwaa  ya vyombo vya habari; ushirikiano katika uwanja wa huduma  za kijamii na diakonia; mawasiliano kati ya wawakilishi wa utawa wa Urusi na Ethiopia na pia uendelezaji wa programu za hija nchini Ethiopia na Urusi.
Picha: Ivan Kharlamov
Shirikisha katika mitandao ya kijamii:

Taarifa zote zilizo na maneno muhimu

-