Mnamo Aprili 25, 2023, Jumanne ya wiki ya pili baada ya Pasaka, Siku ya Radonitsa, Patriarki wa Mosko na Urusi Yote Mtakatifu Kirill aliadhimisha Liturgia Takatifu na kumbukizi ya Pasaka ya marehemu wote, katika kanisa la Malaika Mkuu lililoko Kremlin mjini Mosko, tovuti ya Patriarkia.ru inaripoti.
Mtakatifu Patriarki alihudumu huku akisaidiwa na Askofu Mkuu Tomaso wa Odintsovo na Krasnogorsk, Mkuu wa Sekretarieti ya Utawala ya Patriarkia ya Mosko; Askofu Savva wa Zelenograd, Naibu Afisa Utawala wa Patriarkia ya Mosko; Makasisi wa Mosko.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wa Kikosi-Kazi cha Uratibu wa Mahusiano ya Pande Mbili kati ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi na Kanisa la Malankara: Metropolitani wa Klin Leonid, Askofu Mkuu wa Afrika, Mwenyekiti-Mwenza wa Kikosi-Kazi; Kasisi Mtawa Stefan (Igumnov), Katibu wa DECR MP juu ya Mahusiano kati ya Wakristo, Katibu wa Kikosi- Kazi; Metropolitani Abraham Mar Stephanos, Mkuu wa Dayosisi ya Uingereza, Ulaya na Afrika; Padri Ashwin Fernandis, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Mahusiano ya Nje, ya Kanisa la Malankara.
Maombi maalum yalifanywa kwenye litania maalum, na Mkuu wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi alisoma sala kwa ajili ya Urusi Takatifu.
Katika litania ya mahitaji, maombi yalitolewa kwa ajili ya kupumzika kwa roho za watumishi wa Mungu waliolala – ” Watakumbukwa daima Wakuu wa Kanisa la Urusi, wajenzi na watawala wa Urusi Takatifu, wana wa kifalme, wafalme na malkia, na wale wote waliokuwa madarakani, waliokuwa na jukumu la utunzaji na uangalizi wa imani tukufu ya Kikristo iliyotamalaki katika nchi yetu, mahali hapa walipopumzika mababu zetu, baba na kaka zetu waliozikwa mahali pengine na marehemu wote wa tangu zama za kale, nao tunawakumbuka hivi sasa.”
Katika kuhitimisha Liturgia, Patriarki Mtakatifu Kirill alifanya litania ya mazishi na uvumba kwenye makaburi yaliyoko katika kanisa la Malaika Mkuu lililoko Kremlin.
Kisha Patriarki Mtakatifu aliwapongeza washiriki wa ibada hiyo ya kumbukizi ya Pasaka ya marehemu wote.
Aidha, Patriarki Mtakatifu Kirill aliishukuru kwaya na pia akawakaribisha wajumbe wa Kanisa la Malankara waliokuwa wamewasili Mosko ili kushiriki katika kikao cha Kikosi-Kazi cha Uratibu wa Mahusiano kati ya Kanisa la Kiothodoksi la Urusi na Kanisa la Malankara.Mtakatifu Patriarki akasema: “Napenda kumkaribisha Baba Askofu na padri wanaowakilisha Kanisa la Malankara la India. Ni hakika, kwamba Kanisa hili ni halisi, kwa maana kwamba halijumuishi wageni walifika India kama wamisionari, bali wakazi – asilia ambao mioyoni mwao wamebeba imani ya Uothodoksi kutoka kwa Mtakatifu Tomaso Mtume.
Tunafurahi, ndugu zangu, kwamba Kanisa lenu limedumisha imani kwa milenia mbili sasa, huku likiwaelimisha watu na kuiombea nchi yenu. Watu wa India wako karibu sana na watu wetu, na tunashabihiana kwa mengi, na sasa, kwa neema ya Mungu, tunatembea katika njia nyingi za mwelekeo mmoja katika kukabiliana na changamoto zinazousonga ulimwengu.
Bwana azisaidie Urusi na India, ayasaidie Makanisa, la Urusi na la Malankara, ili yatekeleze huduma zake za kitume, nuru ya Kristo isijefifia katika mioyo na akili za watu wetu.
Karibuni, ndugu wapendwa, ninafurahi kuwaona leo katika Kanisa la Kiothodoksi la Urusi. Kristo amefufuka!”