SALAMU ZA MWADHAMA LEONID, METROPOLITANI WA KLIN, ASKOFU MKUU WA AFRICA, KATIKA HAFLA YA KUZINDUA TOVUTI YA ESARKIA - Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika
RUS | ENG | FRA | SWA | DEU | عرب | Ελλ | PT

SALAMU ZA MWADHAMA LEONID, METROPOLITANI WA KLIN, ASKOFU MKUU WA AFRICA, KATIKA HAFLA YA KUZINDUA TOVUTI YA ESARKIA

Wapendwa!

Azimio la kihistoria la Sinodi Takatifu ya Kanisa la Othodoksi la Urusi, la tarehe 29 Desemba, 2021, juu ya uundaji wa Esarkia ya Kipatriarki ya Africa, lilitoa msukumo mkubwa wa kuthibitisha Uorthodoksi katika bara la Afrika. Katika kipindi cha miezi sita ya uwapo wa Esarkia, wamisionari wa Kanisa la Othodoksi la Urusi wameweza kutembelea nchi kumi na moja za Afrika, wameongoza Liturgia Takatifu, za kwanza, wakihudumu pamoja na makasisi wazawa wa huko, ambao wamehamia na kuwa chini ya mamlaka ya Kiroho ya Mwenye-heri Patriarka Kirill wa Mosko na Urusi yote, na kufanya mazungumzo na. makasisi hao, pia pamoja na waumini.

Nilifanya mikutano yangu ya kwanza na viongozi wa dini na pia wa siasa: Patriarka wa Kanisa la Koptiki Tawadros II, na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni. Naweza kusema kwa uhakika kabisa juu ya mtazamo chanya wa kanisa hilo na wa mamlaka za kiserikali kwa utume wetu, na utayari wao kushirikiana nasi.

Tukio muhimu zaidi na la kihistoria, lilikuwa ni lile la kuongoza Liturgia Takatifu, ya kwanza katika hadhi yangu ya Uaskofu katika ardhi ya Afrika, mnamo tarehe 25Juni mjini Kairo.

Makasisi wa Esarkia katika nchi za Afrika wanaendelea kufanya huduma yao, parokia zinafunguliwa, Liturgia na Ubatizo zifanyika, kazi ya umisionari na katekisti inafanywa, jumuiya mpya zinajiunga na Esarkia.

Leo tovuti ya Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika inaanza kazi yake. Uzinduzi wake utatuwezesha kuwapo kwa uthabiti zaidi katika uwanda wa habari, tukihabarisha kwa wakati-muafaka juu ya matukio muhimu ya shughuli za Esarkia, na kuwajulisha-mubashara wasomaji wetu ulimwenguni kote juu ya utume wa Kanisa la Othodoksi la Urusi barani Afrika. Nina hakika kuwa watakaotembelea tovuti hii wataweza kupata habari kamili na za uhakika juu ya maisha na shughuli za Esarkia changa kabisa ya Patriarkia ya Mosko.

Kanisa la Kikristo, tangu kuanzishwa kwake, limekuwa na utamaduni wa kukumbatia watu wa makabila mbalimbali. Nina hakika kwamba shughuli za mtandao huu zitatumika pia kudhihirisha sababu za kuanzishwa kwa huduma ya uinjilisti wa kanisa katika bara la Afrika na kwingineko.

Pamoja na kuwaombea, ninawatakia wahariri na waandishi wa makala za tovuti, mafanikio katika ubunifu wa kazi itakayozaa “matunda yaletayo uzima wa milele” (Yohana 4:36), na kwa wasomaji wetu – amani, afya na msaada wa Mungu katika kazi zao.

Ninaitia baraka za Mungu juu yenu!

+Leonid
METROPOLITANI WA KLIN,
ASKOFU MKUU WA AFRIKA

Shirikisha katika mitandao ya kijamii: