Mwenyekiti wa Idara ya Misioni ya Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika, Padri Georgi Maksimov, azuru Jamhuri ya Burundi.
Tarehe 14 Januari 2023, katika sikukuu ya Tohara ya Bwana, siku ya kumbukumbu ya Mtakatifu Basil Mkuu, Askofu Mkuu wa Kaisaria ya Kapadokia, LiturgiaTakatifu iliadhimishwa mjini Bujumbura na Padri Georgi Maksimov, makasisi wa Esarkia, mkuu wa parokia nchini Rwanda, Padri Petro Bikamumpaka na Padri Klement Mastaki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ibada hiyo iliendeshwa kwa lugha za Kislavoni cha Kanisa na Kifaransa.
Walioabudu katika Liturgia hiyo ni pamoja na Balozi wa Shirikisho la Urusi katika Jamhuri ya Burundi V. A. Mikhailov, wafanyakazi wa ubalozi, na raia wa Urusi wanaoishi huko pamoja na familia zao.
Katika kuhitimisha, kulifanyika huduma ya sala ya maji matakatifu, kisha Baba Georgi aliwagawia waumini maandiko ya kuelimisha yakiwa katika lugha za Kirusi na Kifaransa.
Makasisi Petro na Klement walitoa hotuba za kukaribisha, huku wakitoa ushuhuda wa raha na furaha yao kuwa katika Kanisa la Kiothodoksi la Urusi.
Baada ya ibada, wakati wa mazungumzo, Warusi wanaoishi Burundi waliwasilisha ombi la kufungua parokia ya Patriarkia ya Mosko nchini Burundi.
Siku hiyo hiyo, Padri Georgi Maksimov alifanya semina ya kichungaji pamoja na mapadri kutoka Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akielezea mipango ya maendeleo ya misioni ya Kiothodoksi. Baadaye Baba Georgi alikutana na Warundi wanaotaka kuwa washiriki wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi.
Siku moja kabla, Padri Georgi Maksimov alikutana na Balozi wa Urusi nchini Burundi, V. A. Mikhailov, ambapo walijadili masuala ya uwepo wa Kanisa la Kiothodoksi la Urusi nchini humo, kwanza kabisa, kuhusu hatua za dhati zinazohitajika katika kurasimisha usajili wa Kanisa serikalini.
“Ninamshukuru Mheshimiwa Balozi wa Shirikisho la Urusi katika Jamhuri ya Burundi, V. A. Mikhailov, kwa msaada wake binafsi, na kwa ushirikiano wa ofisi yake,” Metropolitani Leonid anaandika katika chaneli yake ya mtandao wa “telegram”.