UJUMBE WA KRISMASI
Wa Mtukufu LEONID, Metropolitani wa Klin, Askofu Mkuu wa Africa,
kwa makasisi, watawa na walei wa Esarkia ya Kipatriarki ya Africa
na Dayosisi ya Yerevan-Armenia ya Kanisa la Othodoksi la Urusi
Wapendwa baba, kaka na dada zangu katika Bwana!
Kwa moyo mkunjufu na wa upendo ninawapongeza kwa kuadhimisha sikukuu tukufu ya Kuzaliwa kwa Bwana Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo!
Kanisa la Kiothodoksi sasa linasherehekea ushindi, likilitukuza tukio hili kuu na takatifu sana. Sakramenti ya wokovu, ya kuonekana kwa Mungu katika mwili imetimizwa, na Nuru kuu na ya kweli imeangaza – Kristo Mungu wetu. Ulimwengu umejulishwa juu ya Mungu-Mwana aliyefanyika mwili: Malaika wa Mungu, usiku ule wa Krismasi, aliwatangazia wachungaji wa Bethlehemu “furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote, kwa maana sasa Mwokozi, ambaye ni Kristo Bwana, amezaliwa katika mji.wa Daudi” (Luka 2:10-11). Baada ya kuchukua asili ya kibinadamu, Bwana anaturudisha kwenye ushirika na Baba wa Mbinguni. Watu ambao walipoteza uhusiano wao na Mungu kutokana na dhambi zao wanaunganishwa tena na kupewa fursa ya kupokea zawadi mbalimbali za neema ya Mungu katika Sakramenti Takatifu na sala za Kanisa kama chanzo chenye uhai na kisichoisha maji kwa wale wote wenye kiu ya ukweli wa Kimungu katika njia ya ukuaji wa kiroho na urithi wa uzima wa milele.
Kwa karne nyingi, manabii walitabiri kuhusu kuzaliwa kwa Kristo Mungu-Mwana, kwa uongozi wa roho mtakatifu, wakionyesha kwamba Masihi aliyezaliwa angekuwa Mwokozi wa ulimwengu. Wokovu ulimaanisha kuwasamehe watu kwa kukataa kwao kufuata mapenzi ya Muumba, kuwajulisha njia ya kweli ya utimilifu wa maisha, kurejesha utaratibu wa kuongozwa na Mungu. Wanadamu hawakuweza kutekeleza utume huu mtakatifu kwa kutegemea nguvu zao wenyewe, kwani uovu ulikwishakuwa sehemu ya asili yao. Lakini Mungu, Muumba na Mweza wa yote, hangeweza kuwaokoa wanadamu bila utashi na ridhaa yao, kwani uhuru wa mwanadamu, ambao Bwana Mwenyewe aliuweka katika asili yetu ili kuakisi sura yake, ungekuwa umeingiliwa.
Kuzaliwa kwa Kristo, Kufanyika-mwili kwa Mwana wa Mungu, lilikuwa ni tendo la upendo wa Kimungu usio na ukomo. Baada ya kuweka sheria yake kama msingi wa kuwepo, Mungu anaitekeleza: maisha ya Yesu Kristo yalikuwa udhihirisho-wazi wa upendo usiojua mipaka wala miisho. Usiku wa Krismasi, Mungu aliingia katika maisha ya wanadamu kwa namna ya Mtoto mchanga aliyezaliwa, dhaifu na asiye na ulinzi, aliyezaliwa si katika jumba la kifalme, bali katika hori la ng'ombe. Kuna ukweli mkuu katika picha hii ya Krismasi: si utajiri, nguvu wala uwezo utakaookoa ulimwengu, bali upendo wa Kimungu, katika kutokuwa- kwake na ulinzi kunakozidi nguvu yoyote ya kibinadamu.
Katika simulizi za injili kuhusu Krismasi, kunasemwa kuhusu mamajusi - wahenga wa Mashariki waliokuja Bethlehemu ili kumsujudia Mtoto-Yesu. Na kama vile wanajimu wa kale walivyosafiri safari za mbali kumtafuta Kristo aliyezaliwa, vivyo hivyo nasi ni lazima tufuate njia ya ukweli na uzima inayoelekea kwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa. Kutoka kwenye usiku na giza la nafsi zetu, tunapaswa kwenda kwenye nuru ya nyota ya Bethlehemu, kutoka kwenye baridi na umaskini wa kiroho - kwenye joto-joto na furaha ya upendo wa Kimungu.
Sasa, wakati wa ibada za Krismasi, sisi, kama wachungaji wa Bethlehemu, tunasikia ujumbe na salamu za malaika "Utukufu una Mungu juu mbinguni, amani duniani, na baraka kwa watu wote!" ( Luka 2:14 ). Furaha hii isiyoelezeka inakaa ndani ya mioyo yetu, ikitusaidia kuyavuka magumu na majaribu yote katika maisha, ikitukumbusha kwamba katika huzuni na katika furaha, msaada wa Bwana daima uko karibu nasi, "Mungu yu pamoja nasi" ( Isaya 8 : 10).
Katika sikukuu ya Kuzaliwa kwa Kristo, ninawapongeza ninyi nyote leo, marafiki zangu wapendwa katika Bwana, na kwa sala ninawatakia furaha angavu ya kiroho, msaada wa Mungu usioshindwa katika kutekeleza kazi ya maisha ya Kikristo, nguvu imara, amani na maisha marefu!
LEONID, Metropolitani wa Klin,
Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika.
Kismasi
Mwaka 2022
Mosko