Mtakatifu Patriarki wa Mosko na Urusi Yote Kirill alitoa salamu katika maadhimisho ya “Siku ya Afrika”.
Kaka na dada zangu wapendwa!
Mwaka huu, Mei 25 ni siku ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, ni wakfu kwa “Siku ya Afrika”, ambayo pia inajulikana kama Siku ya Uhuru wa Afrika. Ninakupongezeni sana kwa tukio hili.
Mahusiano kati ya Urusi na Afrika yako katika misingi na kanuni za urafiki, usawa na kuheshimiana. Nchi yetu ilichangia kikamilifu katika kupatikana kwa uhuru wa watu wa Afrika pamoja na uundaji na uimarishaji wa utaifa wao. Inafurahisha kushuhudia kwamba hivi sasa mawasiliano ya kisiasa yanafanyika kwa mafanikio makubwa, ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi unapanuka, na ushirikiano kati ya mabunge ya nchi zetu unaendelea.
Kwa miaka mingi, Urusi na Afrika zimeunganishwa pia na uhusiano mzuri katika nyanja za kiroho na kitamaduni. Kipekee,Wakristo wa dhehebu la Kiothodoksi, wanaotaka kuhifadhi na kudumisha taratibu na kanuni za kidini, pamoja na kulinda uhuru wao wa kuabudu, wamekuwa wakitafuta egemeo katika Kanisa la Kiothodoksi la Urusi. Mnamo Desemba 2021, uamuzi wa kihistoria ulichukuliwa kule Mosko, juu ya uanzishwaji wa Esarkia ya Kipatriarki ya Afrika. Shughuli zake zinatoa mchango mkubwa katika kukuza uhusiano wa kindugu kati ya watu wa Urusi na wa nchi za Afrika, na kuwa na athari chanya katika mahusiano kati ya madhehebu na pia kati ya imani.
Ninawatakia viongozi wote wa nchi pamoja na watu wa Bara la Afrika amani, utulivu na ustawi.
+KIRILL, PATRIARKI WA MOSKO NA URUSI ZOTE